Dhuluma inapotokea, swali si la mtendaji peke yake bali pia la jamii iliyoishuhudia dhuluma hiyo.
Katika Mithali 31:8-9, tunasoma wito wa kusema kwa ajili ya wale wasioweza kujitetea na kuhukumu kwa haki.
Huu ni ukumbusho kwamba imani ya Kikristo haitualiki kuishi kwa kujali wokovu wetu binafsi pekee huku tukipuuza mateso ya wengine.
Tunapowakumbuka waliouawa, dhamiri zetu zinapaswa kutuchochea kuuliza maswali magumu: Je, tulitafuta ukweli? Je, tulisikiliza familia zilizofiwa? Je, tuliheshimu utu wa walioathirika?
Kunyamaza si dhambi katika kila mazingira; wakati mwingine mtu hunyamaza kwa sababu ya hofu, ukosefu wa taarifa au hatari halisi.
Lakini pale ambapo tuna uwezo wa kusaidia kutafuta ukweli kwa njia salama na za haki, hatupaswi kugeuza kutokujali kuwa hekima.
Dhamiri ya Kikristo inahitaji zaidi ya kutosema uongo; inatuita pia kutafuta mema, kutetea walio hatarini na kukataa kushiriki katika udhalilishaji wa wengine.
Ubinadamu wetu haupimwi tu kwa jinsi tunavyowatendea walio hai, bali pia kwa heshima tunayowapa waliopoteza maisha na familia walizoziacha.
UPATANISHO BILA UKWELI NI JENGO LINALOKOSA MSINGI.
Katika maisha ya Kikristo, upatanisho ni zawadi na wajibu. Tunaitwa kujenga upya mahusiano yaliyovunjika na kuondoa chuki zinazotutenganisha.
Lakini upatanisho wa kweli haupaswi kuchanganywa na kufuta kumbukumbu, kuficha ushahidi au kuwashinikiza waliojeruhiwa wanyamaze.
Yesu anasema katika Mathayo 5:23-24 kwamba mtu anapokumbuka kuwa ndugu yake ana jambo dhidi yake, anapaswa kwanza kushughulikia uhusiano huo kabla ya kuendelea na ibada yake.
Fundisho hili linaonyesha kwamba mahusiano na wajibu wetu kwa wengine ni muhimu katika maisha ya kiroho.
Tunapozungumzia vifo vya watu, upatanisho wa kweli unahitaji huruma kwa familia zilizofiwa, utayari wa kusikiliza, uchunguzi wa haki na uwajibikaji pale makosa yanapothibitishwa.
Hakuna anayepaswa kunyimwa haki ya kutafuta ukweli kwa sababu tu wengine wanataka kuendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichotokea.
Kusamehe si kusema kwamba uovu ulikuwa wema. Kupatanisha si kufuta WAJIBU. Na kutafuta haki si lazima kumaanishe kutafuta kisasi.
Tukumbuke waliouawa. Tuheshimu familia zao. Tukatae chuki na taarifa zisizothibitishwa. Lakini pia tusikubali ukimya wa uongo inayotegemea kusahaulisha maumivu badala ya kuyashughulikia.
Upatanisho wa kweli hauogopi ukweli. Unautafuta, unakabiliana nao na kuujenga kuwa msingi wa maisha mapya.
Maisha ya waliouawa mwaka jana yalikuwa na thamani, familia zao zina haki ya heshima, na jamii ina sababu ya kutafuta ukweli.
Uongo hauponyi taifa. Ukweli, haki na uwajibikaji ndivyo vinavyoweza kuanza kuliponya.
Kiongozi si lazima ajue kila kitu kuhusu tukio fulani. Anaweza kukiri kwamba tukio lilitokea. Anaweza kuomba msamaha. Anaweza hata kurekebisha kauli yake baada ya kupata ushahidi mpya.
Hayo si udhaifu. Ni uaminifu.
Tatizo huanza pale ambapo kulinda taswira kunakuwa muhimu kuliko kujua kilichotokea, na pale ambapo maswali ya msingi yanaonekana kuwa maadui badala ya nafasi ya kutafuta haki.
Sifa za mwanadamu ni za muda. Lakini uaminifu ni wajibu wa dhamiri.
Kuna maumivu ya kufiwa na mpendwa. Lakini kuna maumivu mengine yanayoweza kuongezeka pale waliofiwa wanapoona kwamba maswali yao yanapuuzwa au kwamba ukweli unaonekana kuwa tishio kwa wenye mamlaka.
Ndiyo maana uwajibikaji baada ya vifo vya watu ni suala la haki na pia la utu.
Usiwaambie watu wawe na amani kabla hujasikiliza kwa nini wanalia.
Amani ni jambo jema. Umoja wa jamii ni muhimu. Lakini amani ya kweli haiwezi kujengwa kwa kudharau maumivu ya waliofiwa au kuyachukulia maswali yao kama usumbufu.
Katika Injili ya Yohane 11:33-35, Yesu anakutana na Maria, Martha na wengine waliokuwa wakiomboleza kifo cha Lazaro. Yesu anaguswa na huzuni yao, na Injili inasema: “Yesu akalia machozi.”
Hili ni fundisho lenye uzito wa kiroho: mbele ya kifo, huruma si udhaifu. Ni sehemu ya upendo.
Ikiwa Yesu hakudharau machozi ya waliokuwa wamefiwa, sisi ni nani hata tuwadharau watu wanaotafuta majibu kuhusu wapendwa wao?
Viongozi wanapaswa kuelewa kwamba jamii haiwezi kuponya majeraha ambayo hairuhusiwi hata kuyazungumzia.
Kuwasikiliza walioathirika hakumaanishi kuhitimisha mapema kwamba kila madai ni ya kweli. Kunamaanisha kuyachukulia kwa uzito na kuhakikisha kwamba ukweli unatafutwa bila upendeleo.
Amani inayodumu haiogopi maswali. Umoja wa kweli hauhitaji watu wajifanye kwamba hawajaumia. Na upatanisho hauwezi kuwa wa kina ikiwa maumivu ya wahanga yanadharauliwa.
Tuwape waliofiwa nafasi ya kuomboleza. Tuheshimu maswali ya jamii.
ROZARI TAKATIFU, ALHAMISI (MATENDO YA MWANGA)
1. Yesu anabatizwa mto Yordani. - Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo
2. Yesu anageuza maji kuwa Divai huko Kana.
- Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya Injili.
3. Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu.
- Tumwombe Mungu atujalie tupokee ufalme wake kwa toba ya kweli.
4. Yesu anageuka sura.
- Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung'arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.
5. Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristi.
- Tumwoombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine
Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu, Utuombee!
Tunakataa kusahaulishwa yaliyotokea. Tunakataa kulazimishwa kuona ilikuwa jambo la kawaida. Tunakataa unyama uliofanywa ndani ya nchi yetu na wenye mamlaka. Tunakataa wenye nguvu kupuuza maisha ya wanyonge. Tunakataa kusahau damu isiyo na hatia iliyomwagika.
HATUTASAHAU KAMWE!🇹🇿
Tunapowakumbuka waliouawa, hatuitafuti jamii inayotawaliwa na kisasi. Tunaitafuta jamii inayothamini maisha, inayosikiliza waliofiwa na inayokataa kufunika makosa yaliyo wazi.
Amani ya kweli haijengwi kwa kusahau waliopoteza uhai wao. Inajengwa kwa kuhakikisha kwamba maisha yao hayakupotea bila jamii kujifunza, kutafuta haki na kuchukua hatua zinazostahili.
💔🕊️🇹🇿🕯️ Tarehe kama ya leo 29 Oct 2025, risasi na mabomu yalikatisha maisha ya ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi, zikaacha watoto yatima, wazazi wakiwa na vilio na familia zikiwa na maumivu yasiyoelezeka. Wengine walitoka nyumbani bila kujua kuwa hawatarudi tena.
Ee Mwenyezi Mungu, uwapokee ndugu zetu na uwafariji wote waliobaki na majeraha ya kudumu mioyoni mwao. Uhai wa mwanadamu una thamani.
Raha ya milele uwape Ee Bwana, na mwanga wa milele uwaangazie. Wapunzike kwa amani, Amina🙏
SALA YA ASUBUHI
+Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu mmoja, sasa na siku zote na milele amina. Ee utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu; +Baba, +Mwana na +Roho Mtakatifu. Ninasadiki kuwa upo hapa na mahali pote.
Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristu, umenizidishia neema zako, umenitayarishia makao yangu mbinguni.
Ee Mungu wangu, nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda. Ee Mungu wangu, ninakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi na furaha, na mateso yangu, uyapokee unipe neema yako nisitende leo dhambi, Amina.
BABA YETU.
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALAMU MARIA.
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu, mzao wa tumbo lako, amebarikiwa.
Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
KANUNI YA IMANI.
Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia; na kwa Yesu Kristo Mwanae pekee, Bwana wetu, aliyetungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu; siku ya tatu akafufuka kutoka wafu, akapaa mbinguni; ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu Katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, na uzima wa milele. Amina.
AMRI ZA MUNGU.
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu miungu wengine.
2. Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.
3. Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu baba na mama; upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini.
7. Usiibe.
8. Usiseme uongo.
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.
AMRI ZA KANISA.
1. Hudhuria Misa takatifu Dominika na Sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya Jumatano ya Majivu; usile nyama siku ya Ijumaa Kuu.
3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa Pasaka.
5. Saidia Kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.
Ee Maria Bikira Mtakatifu, Mama wa Mungu na Mama yangu, nawe Mtakatifu Yosefu, Nawe Malaika Mlinzi wangi, Nanyi watakatifu somo wangu, nanyi Watakatifu wote, Niombeeni nipate kuacha dhambi, nilindeni siku ya leo na siku zote, na saa ya kufa kwangu, Amina.
MALAIKA WA BWANA
•Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
~Salamu Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
•Ndimi mtumishi wa Bwana, Nitendewe ulivyonena.
~Salamu Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
•Neno wa Mungu akatwaa mwili, akakaa kwetu.
~Salamu Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
Utuombee Mzazi mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.
Tuombe:
Tunakuomba, ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya mtu, kwa mateso na msalaba wake utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu Amina.
SALA KWA MALAIKA MLINZI
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.
Moyo Mtakatifu wa Yesu, Utuombee
Roho za waamini marehemu wapate rehema kwa Mungu wapumzike kwa amani.
+Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Tunapoona watu wanapotea na wengine wanauawa tunapaswa kujiuliza: Je, taasisi zetu zinalinda uhai? Mifumo yetu inaruhusu uchunguzi huru? Watu wanaweza kuuliza maswali bila kutishwa? Wenye mamlaka wanawajika na kuwajibishwa kwa haki?
Wito wa sala. Sala ni silaha!
Kama wewe ni mzazi, usimchape mtoto halafu umwambie hamna kulia. Huo ni udikteta. Kumchapa inaweza kuwa haki yako kwasababu una nguvu au uwezo wa kumchapa, lakini kulia ni haki yake ya msingi kabisa kueleza maumivu yake.
Oktoba 29 watu walichapwa kimwili, kiroho, kihisia, kijamii, kiuchumi nk. Msiwakataze watu hao kulia wakati mliwachapa nyie. Acheni walie.
Neno AMANI lisitumike kuhalalisha uovu. Amani si ukimya wa lazima, ni matunda ya haki inayoheshimu utu wa mwanadamu.
Jamii inaweza kuonekana imetulia kumbe ndani yake kuna maumivu, maswali yasiyojibiwa na familia zinazoishi na huzuni ya kutopata ukweli.
Ndiyo maana ni muhimu sana kutofautisha amani ya kweli na ukimya unaotokana na hofu.
MUNGU HASIKII TAMKO LA VIONGOZI PEKEE, ANASIKIA NA KILIO CHA WAHANGA PIA.
Kiongozi anaweza kusimama mbele ya kamera na kutoa maelezo yake kuhusu yaliyotokea. Anaweza kutumia mamlaka yake kutetea msimamo wake. Lakini kuna jambo ambalo hakuna cheo kinachoweza kulifuta: Mungu anaijua kweli yote.
Katika Biblia, Mungu anasema: “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao” (Kutoka 3:7).
Mungu hakuanza kwa kusikiliza maelezo ya Farao kuhusu utawala wake. Aliona mateso ya waliokuwa wakikandamizwa.
Hili ni fundisho zito kwa kila mwenye mamlaka: usipime haki kwa kile unachotangaza, bali pia kwa kile ambacho walio chini ya mamlaka yako wanakipitia.
Kilio cha familia iliyompoteza mpendwa hakiwezi kufutwa kwa tamko la kisiasa. Huzuni ya mama aliyefiwa haiwezi kutenguliwa kwa hotuba. Na ukweli hauwezi kuamuliwa na sauti yenye nguvu zaidi.
Kama kuna watu waliouawa, wajibu wetu si kushindana katika kutengeneza simulizi zinazotulinda, bali kutafuta ukweli, kuwajibisha wahusika na kuheshimu utu wa kila aliyeathirika.
Mbele ya Mungu, hata sauti iliyonyamazishwa na mamlaka ina thamani.
Kumbukumbu ya wahanga iwe sauti ambayo dhamiri zetu hazitairuhusu kufa.
"Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane yoyote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.
Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida.
Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema." (Kut 22:21-27)
Kesho 29 Oct tutawakumbuka wenzetu WALIOUAWA KIKATILI baada ya uchaguzi wa Mwaka jana. Hatupaswi kuwasahau ndugu, jamaa na marafiki zetu.
Kumbukumbu yao iwe wito wa ukweli. Maumivu yao yawe wito wa haki. Na kamwe dhamiri zetu zisikubali amani inayojengwa juu ya kukana ukweli.
KUWAKUMBUKA WALIOUAWA NI KUKATAA KUZIKWA KWA UKWELI PAMOJA NAO.
Kila uhai wa mwanadamu una thamani mbele za Mungu. Mtu anapouawa, si familia yake pekee inayopoteza; jamii nzima hupoteza sehemu ya utu wake. Ndiyo maana kuwakumbuka waliopoteza maisha yao si suala la hisia au siasa tu, bali pia ni wajibu wa kimaadili na wa kiroho.
Kinachoumiza zaidi baada ya vifo si kifo chenyewe pekee, bali pia pale ukweli unapofunikwa, ushahidi unapopuuzwa, na wenye mamlaka wanapochagua kukanusha badala ya kutafuta ukweli. Mamlaka hayampi mtu haki ya kuamua ukweli; yanampa wajibu mkubwa zaidi wa kuutafuta, kuuheshimu na kuusema.
Kibiblia, Mungu anauliza: “Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi” (Mwanzo 4:10). Hii inatukumbusha kwamba damu ya asiye na hatia si jambo linalopotea mbele za Mungu kwa sababu tu wanadamu wameamua kunyamaza.
Kwa mtazamo wa Kikristo, kukanusha ukweli wa vifo, pale ukweli huo unapojulikana, si kosa la mawasiliano tu bali ni jeraha jingine kwa haki na kwa utu wa marehemu. Ukweli hauwi uongo kwa sababu umekataliwa na mwenye mamlaka, na haki haikomi kuwa haki kwa sababu imekuwa na gharama za kisiasa.
Yesu alisema: “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32). Taifa haliwezi kuponya majeraha yake kwa kulazimisha kusahaulisha yaliyotokea. Uponyaji wa kweli huanza pale ukweli unapokubaliwa, wahanga wanapotambuliwa, na haki inapofuatwa bila upendeleo.
Maana mbele ya Mungu, cheo si kinga dhidi ya ukweli, mamlaka si ruhusa ya kuunyamazisha, na kusahaulika kwa mhanga hakumaanishi kwamba haki yake imekoma kuwepo.
“Jifunzeni kutenda mema; takeni haki; wasaidieni walioonewa.” (Isaya 1:17)
ROZARI TAKATIFU MATENDO YA UTUKUFU (Jumatano na Jumapili)
1. Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.
2. Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.
3. Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.
4. Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.
5. Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema








